RC MRINDOKO ATOA TAARIFA YA MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA KATIKA MKOA WA KATAVI
Posted on: July 2nd, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Mkoa wa Katavi kwa kasi na mafanikio makubwa katika sekta zote muhimu.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Julai 3, 2025, jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, RC Mrindoko amesema kuwa takribani Shilingi bilioni 58.1 zimetumika kuboresha miundombinu ya elimu. Katika kipindi cha miaka minne, shule mpya za msingi zimeongezeka kutoka 196 hadi 293, huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka 39 hadi 79. Aidha, zaidi ya madarasa 2,200 na matundu ya vyoo 2,700 yamejengwa, sambamba na ongezeko la walimu wapya zaidi ya 900.
Katika sekta ya afya, amesema Serikali imetumia Shilingi bilioni 41.2 kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati mpya. Upatikanaji wa dawa muhimu umefikia asilimia 94, na vituo vinavyotoa huduma za dharura kwa mama na mtoto vimeongezeka kutoka 8 hadi 14.